Jumamosi 12 Aprili 2025 - 11:45
Ayatollah al-Udhma Makarem Shirazi: Mawahabi hawana uwezo wa kutosha wa kielimu kuchambua masuala ya Kiislamu

Hawza/ Hadhrat Ayatollah al-Udhma Makarem Shirazi ameweka wazi kuwa: Mawahabi, kutokana na kukosa uwezo wa kina wa kielimu katika kuchambua masuala ya Kiislamu hususan masuala ya tauhidi na ushirikina wamepatwa na wasiwasi wa ajabu kuhusu masuala haya, na kila walipokutana na jambo lolote la kutatanisha, wanalipinga vikali, miongoni mwa mambo haya ni masuala ya ziara na shifaa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Hawza: Ayatollah Makarem Shirazi katika andiko maalum alilolitoa kuhusu "mawahabi na uharibifu wa majengo ya kihistoria ya kiislamu, na kujibu swali linalosema: Kwa nini mawahabi wanakataa kujengea makaburi?", alijibu kwa ujumla na kwa kina kama ifuatavyo:

Jawabu la ujumla:
Mawahabi, kutokana na uelewa wao finyu kuhusiana na tauhidi pamoja  na shirki, walihukumu kuwa kuruzuru makaburi, kutaka uombezi, kuyajengea, na mambo mengine yanayofanana na hayo ni kinyume cha sheria za kiislamu. Walivihusisha vitu hivyo na shirki na uzushi, na wakavipinga vikali. Mwaka 1344 Hijria, walipopata madaraka katika eneo la Hijazi, kwa kisingizio cha kuondoa uzushi walivunja na kuharibu majengo yote ya kihistoria ya Kiislamu. Urithi huo ulikuwa unakumbusha sehemu muhimu ya historia tukufu ya kiislamu

Jawabu kwa kina:
Mawahabi, kutokana na ukosefu wa uwezo wa kutosha wa kielimu katika kuchambua masuala ya Kiislamu hasa kuhusu dhana ya tauhidi na shirki wamejawa na hali ya wasiwasi usio wa kawaida kuhusu masuala haya. Kila walipopata kisingizio, walijitokeza kupinga. Masuala kama ziara ya makaburi, uombezi, ujenzi juu ya makaburi na mambo yanayofanana nayo yote waliyahukumu kuwa kinyume cha sheria za dini, na wakayahusisha na shirki au bid’ah, hivyo wakayapinga vikali. Miongoni mwa mambo muhimu zaidi waliopinga ni kuyajengea makaburi ya watu mashuhuri katika dini.

Hadi leo hii, katika ulimwengu wa Kiislamu isipokuwa Hijazi majengo makubwa yamejengwa juu ya makaburi ya manabii wa kale na viongozi wakuu wa Kiislamu katika nchi mbalimbali, na zote hizi ni kumbukumbu muhimu za kihistoria. Kuanzia Misri hadi India, na kutoka Algeria hadi Indonesia, watu wanaziheshimu sana athari za kiislamu zilizopo katika nchi zao na wanathamini kwa dhati makaburi ya watu mashuhuri wa dini.

Lakini katika Hijazi hakuna hata dalili ya mambo haya. Kwa nini? Sababu kuu ni ukosefu wa uelewa sahihi na uchambuzi makini kuhusu dhana za msingi za Kiislamu.

Karne moja iliyopita, tukio la kuhuzunisha lilitokea katika ardhi ya wahyi (Makka na Madina), ambalo liliwafanya Waislamu wakose kabisa athari za kihistoria za kiislamu. Tukio hilo lilikuwa ni mawahabi kupata madaraka. Takriban miaka 80 iliyopita (mwaka 1344 Hijria), mawahabi walipopata madaraka huko Hijazi, walivunja na kuharibu kabisa majengo yote ya kihistoria ya Kiislamu, wakayafanya sawa na ardhi kwa kisingizio cha kuondoa shirki na uzushi.

Hata hivyo, hawakuthubutu kuharibu kaburi tukufu la Mtume Muhammad (s.a.w), kwa kuogopa kwamba Waislamu wote wangesimama dhidi yao. Kwa namna fulani, kundi hili lililokuwa likikataa "taqiyya", walilazimika kuitekeleza dhidi ya Waislamu wengine kwa ajili ya kujiokoa!

Kwa kila hali, uhai wa jamii yoyote umefungamana na mambo mbalimbali, mojawapo ikiwa ni kuhifadhi urithi wa kiutamaduni, kielimu na kidini. Lakini kwa masikitiko makubwa, ardhi ya wahyi, hasa Makka na Madina, iliwekwa mikononi mwa kundi dogo la watu waliokuwa na mitazamo finyu, ya nyuma kifikra, na wenye msimamo mkali, na kwa sababu ya visingizio visivyo na msingi, urithi muhimu mno wa kiislamu ulipotezwa. Kila sehemu ya urithi huo ilikuwa ni kumbukumbu ya sehemu muhimu ya historia ya uislamu.

Haikutosha kwamba makaburi ya Maimamu na watu mashuhuri waliozikwa Baqii yaliharibiwa, bali pia kila mahali walipokuta athari yoyote yenye thamani ya kihistoria ya Kiislamu waliiangamiza. Tukio hili lilileta hasara kubwa isiyoweza kurekebishwa kwa Waislamu.


Athari hizi za kihistoria zilikuwa na mvuto wa kipekee, na zilikuwa zikimfanya mtu afahamu historia ya uislamu. Makaburi ya Baqi’, ambayo zamani yalikuwa na mandhari ya kuvutia na kila kona yake ikikumbusha tukio muhimu la kihistoria, leo hii yamegeuka kuwa jangwa lenye sura mbaya na ya kusikitisha, na yapo katikati ya hoteli za kifahari na majengo ya kuvutia yenye mapambo mengi. Milango yake ya chuma isiyo ya kupendeza hufunguliwa kwa saa moja au mbili tu kwa siku, na hata hivyo ni kwa wanaume pekee!

Maoni yako

You are replying to: .
captcha